TANZANIA INA UMEME WA KUTOSHA – DKT.BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema hivi sasa Tanzania  ina umeme wa kutosha  hatua ambayo imechangiwa na kukamilika kwa  Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP ) ambao pekee  unazalisha Megawati 2115.

Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Julai 10, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya  Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II ambapo amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO yapo baadhi ya maeneo yalikua na changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.

Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amefafanua kuwa  ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme  katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000 mpango wa sasa.

‘’Nataka niseme  mbele yenu ndugu zangu, Mhe. Rais Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote  yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii imepata  Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa anataka wananchi wapate umeme wa uhakika,’’ alisema Dkt Biteko.

Aidha, Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.

‘’Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto  za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ alisisitiza Dkt. Biteko.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko  aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya nishati  Mha. Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo na  Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange.







Comments